Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, jana tarehe 16.03.2020 imegawa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na walemavu, mikopo ambayo itawasaidia katika kuinua biashara zao na kipato cha kuendesha maisha. Vikundi vilivyopatiwa mikopo vilikuwa na jumla wa watu 85 (wanawake 60, vijana 20 na walemavu 5) na kiasi cha fedha kilichotolewa kwa vikundi hivi vitatu ni Tshs. Milioni sabini na nne, laki tatu na tisini na sita elfu.
Akisoma taarifa ya ugawaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Bi. Mariana Sumari alisema, toka mwaka 2016 mpaka 2020, Halmashauri ya Mwanga, imeshatoa mkopo wa kiasi cha Tsh. Milioni 296.1 kwa vikundi vya wanawake, vijana na walemavu.
Zoezi hilo la ugawaji wa mikipo liliongozwa na Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Ndg. Thomas Apson. Mhe. Apson aliwaasa wanufaika wa mkopo huo kuwa, wahakikishe kuwa wanazitumia fedha hizo vizuri ili waweze kurejesha. Pia aliwahakikishia kuwa, wakirejesha vizuri, wataendelea kupatiwa mkopo zaidi. Mhe. Mkuu wa Wilaya alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri kwa jitihada zake nzuri za kuhakikisha kuwa anawajali wanawake, vijana na walemavu, kwani amefanya jambo nzuri la kuhakikisha kuwa, kila mwaka anatenga fedha kwa ajili ya kukopesha makundi hayo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Ndg. Zefrin K. Lubuva, alitumia fursa ya kuongea na wanakikundi hao na kuwaeleza kuwa, Halmashauri ina fedha nyingi kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu hivyo, vikundi mbalimbali vinasisitizwa kuomba mkopo ili waweze kujikwamua kimaendeleo.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa