•DC awaasa wafanya biashara wadogo kuchukua kwa wingi,
•Asema, watakuwa huru kufanya biashara.
Zoezi la ugawaji wa vitambulisho kwa wafanya biashara wadogo katika Wilaya ya Mwanga limeanza leo ambapo, wafanya biashara kutoka sehemu mbalimbali za Wilaya ya Mwanga wamefika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho hivyo.
Akizungumza akiwa ofisini kwake, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Mhe. Aaron Y. Mbogho amesema, katika Wilaya ya Mwanga, zoezi la kuwabaini wafanya biashara wanaostahili kupatiwa vitambulisho hivyo, lilianza tarehe 24/12/2018, na leo zoezi la kuvigawa limeanza rasmi. Amesema kuwa, Wilaya ina jumla ya vitambulisho 1500 na watavigawa kwa wafanyabiashara wadogo wote watakaokuwa wana sifa ya kupatiwa. Ameendelea kusema kuwa, zoezi hili litakuwa ni endelevu na lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa, kila anayestahili anapatiwa kitambulisho.
Aidha, Mhe. Mkuu wa Wilaya amesema, dhamira kubwa ya Serikali kwa wafanyabiashara wadogo ni kunyanyua kipato chao kwa kuhakikisha wanaondokana na adha ya kulipa ushuru na kodi ambazo haziendani na kipato chao. Amesema, kitambulisho atakachpatiwa mfanya biashara kitamsaidia kufanya biashara mahali popote ndani ya Tanzania pasipo kupata usumbufu wowote. Hivyo amewataka wafanya biashara wadogo waliopo Wilayani Mwanga, na wenye sifa kufika ofisini kwake kwa ajili ya kupatiwa huduma hiyo.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa