Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, leo wamekabidhiwa Lori jipya na Guta jipya. Makabidhiano hayo yamefanywa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Bi. Mwajuma A. Nasombe. Tukio hilo la makabidhiano limefanyika wakati wa mkutano wa Baraza la Madiwani, lililo fanyika leo tarehe 19.05.2023, katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Mwanga, kwa ajili ya kujadili taarifa za kipindi cha robo ya tatu.
Wakati wa makabidhiano hayo, Mkurugenzi wa Halmashauri Bi. Nasombe amesema kwamba, “Lori hili pamoja na guta tumenunua kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri, na ifahamike kwamba, pamoja na shughuli zingine, lori litatumika kama sehemu ya kuongeza mapato ya Halmashauri yetu”, alisema Mkurugenzi Mtendaji. Ameendelea kusema kuwa, Halmashauri ya Mwanga ina mchanga mwingi, hivyo lori lililo nunuliwa litatumika kwa ajili ya shughuli za mchanga wa biashara na mchanga huo utauzwa kwa Halmashauri zilizopo jirani na Wilaya ya Mwanga.
Kwa upande wa Guta, Mkurugenzi amesema, guta litatumika kwenye shughuli mbalimbali za usafi wa mji wa Mwanga. Mji wa Mwanga unahitaji kuwa na vifaa vya usafi na moja wapo ya vifaa vya kusaidia katika usafi ni pamoja na kuwa na usafiri wa kusomba taka, hivyo guta hili litapunguza changamoto iliyo kuwepo, alisema Mkurugenzi.
Naye akipokea lori na guta hilo kwa niaba ya Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Mhe. Dr. Salehe R. Mkwizu amesema kwamba, amefurahishwa sana kwa jitihada zilizofanywa na Waheshimiwa Madiwani pamoja na timu ya Menejimenti ya Halmasahuri kwa kuhakikisha kwamba, wanabuni mradi mzuri, ambao utakwenda kuiingizia Halmashauri mapato kwa njia ya kusambaza mchanga katika Wilaya za jirani kupitia lori hilo. Ameongeza kwamba, lori hilo litasaidia pia katika kurahisisha upatikanaji wa huduma kwenye miradi mbalimbali ya Halmashauri.
Tukio hilo la makabidhiano ya Lori na Guta lilishuhudiwa na Mbunge wa Jimbo la Mwanga Mhe. Joseph Anania Tadayo, ambaye pia aliweza kushiriki katika mkutano wa Baraza la Waheshimiwa Madiwani. Mhe. Mbunge ametoa pongezi kwa uongozi wa Halmashauri kwa ununuzi wa lori hilo na kutoa rai kwamba, Halmashauri ihakikishe inalitunza vizuri na litumike kwa uangalifu.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa