Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga kwa kushirikiana na asasi isiyo ya serikali NAFGEM (Networking Against Female Genital Mutilation) inafanya zoezi la kutoa elimu ya kijinsia mashuleni mahsusi juu ya unyanyasaji wa watoto.
Elimu ambayo inatolewa kwa watoto ni pamoja na haki za watoto kwa mujibu wa katiba na sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Elimu hii inafaida kubwa kwa watoto, kwani wanapata kufahamu haki zao ikiwa ni pamoja na, haki ya kulindwa, kuishi, kusoma, kucheza, lishe bora, malazi bora, kupatiwa matibabu nk. Watu muhimu wa kuwapatia watoto haki zao ni wazazi/walezi pamoja na walimu na haki zote hizi inatakiwa watoto wazipate wakiwa mahali popote kama mazingira ya shule na nyumbani.
Katika kuhakikisha kuwa zoezi hili linafanyika kwa ufanisi wadau mbalimbali wameweza kushirikishwa kwenye mafunzo hayo. Wadau walioshirikishwa ni pamoja na Mkuu wa Wilaya, Kamanda wa Polisi, Polisi Dawati la Jinsia na Watoto, Mwanasheria wa Halmashauri, Maafisa Elimu Shule za Msingi na Sekondari, Mganga Mkuu wa Wilaya, Mratibu wa Afya ya Uzazi, Afisa Ustawi wa Jamii, Afisa Maendeleo ya Jamii, Waratibu wa Afya Shuleni na Watendaji wa Kata za Kirya, Mgagao, Toloha na Lang’ata.
Zoezi hili la kutoa elimu kwa wanafunzi lilianza tarehe 19 Machi, 2018 katika shule ya msingi Mramba na litaendelea kwa shule zote za msingi za wilaya ya Mwanga. Hadi kufikia siku ya tarehe 20 Machi, 2018 shule za msingi Mramba, Mwangondi na Mwanga zilishapatiwa mafunzo ambapo mafunzo hayo yametolewa kwa jumla ya wanafunzi 1313.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa