Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Mhe. Abdallah Mwaipaya, amewakaribisha wananchi wa Wilaya ya Mwanga na wananchi wa Wilaya jirani kushiriki kwenye mapokezi ya kumpokea na kumkaribisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango atakapokuwa kwenye ziara ya kikazi Wilayani Mwanga tarehe 21 Machi, 2024.
Mhe. Mwaipaya ameyasema hayo leo tarehe 15.03.2024 alipokuwa katika ziara ya kikazi ya kusikiliza kero za wananchi wa kijiji cha Kagongo kata ya Lang’ata Bora. Amesema kwamba, Makamu wa Rais anategemea kutembelea na kukagua hatua ulipofikia mradi wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe pamoja na kuongea na wanachi wa Wilaya ya Mwanga katika eneo la stand mpya. “Nitumie nafasi hii kuwaalika na kuwakaribisha wanachi wote wa wilaya ya Mwanga na wananchi wa wilaya jirani kwenye mapokezi ya kumpokea Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atakapo tembelea wilaya yetu tarehe 21.03.2024”, Alisema Mhe. Mwaipaya.
Sambamba na hilo, Mhe. Mkuu wa Wilaya pia amewakaribisha wananchi wa Wilaya ya Mwanga kwenye sherehe za kuwasha Mwenge wa Uhuru zitakazofanyika katika uwanja wa Ushirika – Moshi tarehe 02 Aprili, 2024. Akiwahutubia wanachi wa kijiji cha Kagongo, Mhe. Mwaipaya alisema kuwa, baada ya sherehe za uzinduzi wa Mwenge wa Uhuru, utakimbizwa Halmashauri zote za Mkoa wa Kilimanjaro na Mwenge wa Uhuru utaingia Wilayani Mwanga tarehe 07 Aprili, 2024. Katika hotuba yake kwa wananchi hao, alisema kwamba, wananchi wa Mwanga huwa ni washiriki wazuri sana kwenye sherehe zote za Mwenge wa Uhuru, kwa kila mwaka, hivyo anawaalika kushiriki katika matukio yote mawili ambayo ni sherehe za uzinduzi na sherehe za kukimbiza pamoja na kukesha na Mwenge Wilayani Mwanga tarehe 07 Aprili 2024.
Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mwanga imekuwa ikifanya ziara za mara kwa mara. za kuwatembelea wananchi wake, na kusikiliza kero zao pamoja na kuzipatia utatuzi. Ziara hizi zimekuwa za manufaa makubwa kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuokoa gharama kubwa za kufika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa ajili ya kuwasilisha kero zao.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa