Kaimu Mkuu wa Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika Ndugu Hassan M. Msuya ametoa wito kwa wananchi wa Mwanga kuhakikisha kuwa, wanatumia msimu huu wa mvua kupanda mazao kwa ajili ya kupata chakula cha kutosha ili kuepukana na njaa ya baadae.
Akizungumza akiwa ofisini kwake Ndugu Mamboleo amesema, katika kuhakikisha kuwa wananchi wa Mwanga hawapati uhaba wa mbegu za mahindi, alizeti na muhogo, Halmashauri kwa kushirikiana na taasisi ya utafiti ya Seliani, wameweza kupata mbegu nzuri zinazohimili hali ya hewa na wananchi wanahamasishwa kufika ofisi za kilimo ili waweze kupatiwa mbegu hizo kwa bei nafuu. Kiasi cha mbegu za mahindi zilizopokelewa ni tani 4, hadi sasa zimeshanunuliwa tani 2 ½ na zimebaki tani 1 ½. Amesema kwa sasa mtawanyiko wa mvua upo wilaya nzima ya Mwanga na atashangaa sana kuona wananchi wanaojihusisha na kilimo kama watakuwa hawazitumii mvua hizi za masika vizuri.
Sambamba na kuhakikisha kuwa wanapanda mazao, amewasisitiza wananchi kuhakikisha wanapiga dawa kwenye mashamba yao mara kwa mara kwani kuna aina mpya ya viwavijeshi ambavyo ni hatari sana kwa mazao na endapo wakulima hawatapiga dawa, basi watambue kuwa watavuna chini ya kiwango, ama wasivune kabisa. “Wananchi wabadilike kifikra kwa kuhakikisha wanapiga mazao dawa.”alisema Ndugu Msuya. Akiainisha aina ya viwatilifu vinavyofaa kwa mazao alisema wakulima watumie viwatilifu aina ya Dasban, Duduba na Duduol sambamba na kuhakikisha shamba lenye mazao linafanyiwa usafi mara kwa mara.
Akizungumzia kuhusu maandalizi ya sherehe za nanenane kwa mwaka 2018 Ndugu Msuya amesema kwa sasa Halmashauri imeshaanza maandalizi ya awali na maandalizi haya yanakwenda hatua kwa hatua. Kwa sasa Idara imeshaanza kuandaa vipando kwenye eneo la maonyesho ambalo lipo katika viwanja vya nane nane Arusha. Ifikapo tarehe za mwishoni za mwezi machi na mwezi aprili, zoezi la kushindanisha wakulima kwa ngazi ya kijiji, kata, wilaya na mkoa itakuwa imefanyika ili kupata wakulima wazuri watakaoshirikishwa kwenye maonyesho ya nane nane.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa