Wananchi wa Kijiji cha Karambandea ambacho kipo kata ya Toloha Wilayani Mwanga, wameanza kunufaika na mradi wa shirikika la kimataifa la WWF shirika linalo jihusisha na uhifadhi wa wanyama pori na mazingira. Shirika la WWF limeanza mradi wake wa utafiti wa simba katika ukanda wa Tarafa ya Jipendea hususani katika kijiji cha Karambandea, kijiji ambacho kipo karibu kabisa na mbuga ya wanyama pori ya mkomanzi na mbuga jirani ya Tsavo Kenya.
Sambamba na uanzishwaji wa mradi huu, miongoni mwa manufaa ambayo mradi umeleta na unategemea kuendelea kuleta kwa wananchi wa Karambandea ni pamoja na ujenzi wa maboma ya kisasa ya kulaza mifugo ili isidhuriwe na wanyama aina ya paka kama simba, chui,duma, fisi nk. Manufaa mengine ambayo wananchi wa kijiji hicho wameanza kunufaika nayo ni mradi wa umeme wa sola ambapo mradi huu utasaidia katika kudhibiti na kupambana na wanyama wakali. Pia mradi umeanza kuleta manufaa kwa jamii hii kwa kuweza kujengewa Bwawa la kunyweshea mifugo, bwawa ambalo litakuwa msaada mkubwa wakati wa kiangazi.
Msimamizi wa mradi huo wa simba ambaye anahusika na usimamizi upande wa Tanzania na Kenya Prof.Noah Sitati ambaye alishiriki katika ziara ya kuuzindua mradi huo alisema, mradi huu utasaidia wanyama pori kuongezeka na watalii wataingia kwa wingi kupitia wilaya ya Mwanga. Pia mradi utawezesha kufunguliwa kwa lango la utalii kwa upande wa wilaya ya Mwanga kwenda mbuga ya wanyama ya Mkomanzi. Prof. Sitati pia amesema, hapo baadae mradi utawezesha kuanzishwa kwa miradi ya kuboresha nyasi kwa ajili ya malisho ya mifugo.
Naye Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Ndg. Abdllah Mwaipaya, amelishukuru shirika la WWF kwa mpango wake mzuri wa kuja na mradi wa utafiti wa simba hapa Wilayani Mwanga kwani eneo la Karambandea lina mgongano mkubwa na wa mara kwa mara kati ya wanyamapori na binadamu. Ameendelea kusema kwamba, mradi huo utasaidia utunzaji wa mazingira kwa asilimia kubwa, pamoja na kuinufaisha jamii ya wafugaji wa Karambandea na Tarafa ya Jipendea kwa ujumla.
Mhe. Mwaipaya pia ameishukuru jamii ya wananchi wa Karambandea kwa kukubali kupokea mradi huo kwani wananchi wa kijiji hicho wamekuwa wakikataa miradi mingi kutokana na uelewa mdogo waliokuwa nao awali kuhusu miradi. Amesema, wananchi hao kwa sasa wamepatiwa elimu vizuri na wameshaanza kuelewa umuhimu wa miradi katika maeneo wanayoishi.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa