Katika kuhakikisha kuwa mwananchi wa Mji wa Mwanga anapata huduma nzuri ya maji na ya kiwango chenye tija Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanga Mjini imeandaa rasimu ya mkataba wa huduma kwa mteja, rasimu ambayo kwa hatua za awali imeshawasilishwa EWURA na sasa imeletwa kwa wananchi ili waione, waisome na kuijadili na baade irudishwe EWURA kwa hatua zaidi.
Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Ndg. Aaron Y. Mbogho ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi wakati wananchi wa mji wa Mwanga wakisomewa rasimu hiyo alisema ameipitia rasimu na ameiona ni nzuri ila anaomba wananchi ambao ndio wadau wa maji waweze kuipitia na kama kuna chochote cha kuongezea basi kitatoka kwa wadau wa maji.
Akiwasilisha rasimu hiyo kwa wananchi wa mamlaka ya mji wa Mwanga, Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanga Mjini Bi. Stellah Shija alisema rasimu ya mkataba huo ni nzuri kwasababu, imebeba mambo mbalimbali ambayo yatamnufaisha mteja ikiwa ni pamoja na mamlaka kujikita kwenye kuhakikisha kuwa, inatoa huduma nzuri ya maji, kusambaza matawi, kurekebisha miundombinu, kusikiliza kero za wateja, usomaji wa dira za maji, uzalishaji na usambazaji wa maji, kuzifanyia matengenezo dira za maji sambamba na kuhakikisha haki za mteja zinazingatiwa.
Akiendelea kuwasomea na kuwaelimisha wananchi wa Mji wa Mwanga juu ya rasimu hiyo, Bi. Shija alisema, rasimu inampa mteja haki ya kupewa fidia pale mamlaka ya maji itakaposhindwa kufikia malengo ya utoaji wa huduma kwa mteja na hii ni kwa mujibu wa kanuni ya mwaka 2016 ya usambazaji wa maji safi na usafi wa mazingira (ubora wa utoaji wa huduma). Akiainisha fidia hizo alisema fidia halisi zitaanzia Tsh. 10,000 na fidia ya juu itakuwa Tsh.40, 000 na hii itategemea na aina ya huduma ambayo haikutolewa kwa wakati huo. Fidia hii itatolewa pale tu ambapo lengo la utoaji wa huduma litakuwa halikupata kutekelezwa kwa wakati.
Bi. Shija alieleza kuwa pale ambapo mamlaka ya maji itachunguza malalamiko ya mteja na kugundua kuwa kuna kasoro zimejitokeza mteja atapewa fidia ya gharama zisizo za kifedha na mteja ataombwa msamaha kwa maneno na maandishi, mteja atapewa huduma aliyostahili siku hiyo hiyo baada ya mamlaka kugundua kulikuwa na kasoro. Mteja pia anaweza kudai fidia ya fedha alizotumia kama gharama za usafiri, posta, simu au madai mengine yenye uthibitisho unaokubalika kwenye kanuni za fedha. Aidha amesisitiza kuwa fidia zote zitakazobainika na kutakiwa kulipwa hazitakuwa fedha taslim ispokuwa kwa kuweka kumbukumbu ya malipo (credit transaction) kwenye akaunti ya mteja ya malipo ya huduma ya maji safi.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa