Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga kwa kushirikiana na shirika la Msalaba Mwekundu (Red Cross), wameendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na virusi vya Corona.
Zoezi hili ambalo lilianza jana tarehe 27.07.2020 linategemea kumalizika tarehe 30.07.2020 ambapo jumla ya Tarafa 5 na kata 20 zitakuwa zimepitiwa.
Lengo kubwa la kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya ugonjwa wa Covid 19 ni kuwakumbusha na kuwataka wananchi kuendelea kuchukua taadhari dhidi ya ugonjwa huo kwa kuhakikisha kuwa wananawa mikono mara kwa mara, kuepuka safari zisizo za lazima, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kuvaa barakoa pamoja na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.
Sambamba na hilo, wananchi wameendelea kukumbushwa kuwa, waonapo dalili za Covid 19, wasiache kuhudhuria kwenye kituo cha afya mara moja ili kupima afya. Pia wameendelea kupewa elimu juu ya dalili za Covid 19 ikiwa ni pamoja na mwili kuchoka, mafua makali, homa, kukohoa mara kwa mara, kichwa kuuma pamoja na kupumua kwa shida.
Aidha, elimu hii imepita kwenye maeneo yote yenye mikusanyiko ya watu kama masoko, maduka ya biashara, taasisi mbalimbali za Umma na binafsi kama shule na vyuo. Elimu hii imetolewa kwa njia ya kugawa na kubandika mabango, kutumia vipaza sauti, kupita shuleni na kuongea na wanafunzi pamoja na walimu wao, kuongea na wananchi sehemu zenye mikusanyiko kama sokoni na vijiwe vya bodada.
Maeneo ambayo yameshapitiwa mpaka sasa ni pamoja na kata za Kileo, Lembeni, Lang'ata, Kirya, Kighare, Kirongwe, Chomvu, Msangeni, Kifula, Kwakoa, Toloha, Kigonigoni, Jipe na Kivisini na maeneo yaliyosalia yatapitiwa tarehe 29-30 Julai, 2020.
Pamoja na haya wananchi mnaendelea kukumbushwa kuwa, ugonjwa wa Corona hapa Tanzania umepungua sana. Pamoja na hayo, tunapaswa kuendelea kuchukua taadhari na kuzingatia maelekezo yanayotolewa mara kwa mara na wataalamu wa afya, pia tuhakikishe kuwa, tunafuatilia na kusikiliza vyombo vya habari.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa