Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amewaahidi wananchi wa Wilaya ya Mwanga kuwa, wategemee kupata maji ya kutosha kutoka kwenye mradi mkubwa wa maji wa Mwanga - Same - Korogwe. Aliyasema hayo wakati alipotembelea mradi huo hapo jana na kujionea namna shughuli za mradi zinavyoendelea kuanzia sehemu ya chanzo cha mradi pamoja na sehemu ya kutibu maji.
Mradi wa Mwanga - Same - Korogwe ni mradi ulioanza toka Desemba, 2014 na sasa umefikia asilimia 64%. Akieleza sababu za kuchelewa kwa mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 262, Mhe. Waziri Mkuu alisema, ili mradi huo ukamilike unapitia hatua nne ikiwa ni pamoja na hatua ya kutengeneza chanzo, kutengeneza eneo la kutibu maji, kujenga visima na kulaza mabomba kwaajili ya kusambaza maji. Kutokana na kazi za maeneo haya manne kuwa kubwa, imechangia mradi kuchelewa kukamilika.
Katika hotuba yake, Mhe. Waziri Mkuu pia hakuacha kusemea vijiji ambavyo mradi umeanzia pamoja na vijiji ambavyo mradi utapita. "Wasimamizi wa mradi wahakikishe kuwa, vijiji vyote ambavyo vipo kwenye chanzo cha mradi pamoja na vile vijiji ambavyo mabomba yatapita vipatiwe maji" alisema Waziri Mkuu.
Mradi wa Mwanga - Same - Korogwe ni mradi mkubwa wa kimkakati, wenye thamani ya shilingi bilioni miambili sitini na mbili. Mradi huu utakuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi zaidi ya 438,000 wa Wilaya za Mwanga, Same na Korogwe na utakuwa na uwezo wa kutoa maji masaa ishirini na nne kila siku.
Aidha, katika ziara yake hiyo, aliweza kukutana na mkandarasi aliyekuwa akisimamia mradi, mkandarasi ambaye mkataba wake ulivunjwa mwanzoni mwa mwaka huu. Mhe. Waziri Mkuu alimwagiza Waziri wa Maji kuwa, mkandarasi huyo arudi kazini ili aendelee na kazi na kumtaka mkabdarasi huyo aendelee na kasi ili mradi ukamilike mapema.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa