•NDOO 150 ZAKAMATWA
•MAGARI 2 NA PIKIPIKI 2 ZASHIKILIWA
Huku kukiwa bado kuna zoezi la operesheni ya uvuvi haramu katika bwawa la Nyumba ya Mungu, bado kuna baadhi ya wavuvi na wafanya biashara ambao wanajihusisha na shughuli za uvuvi haramu na biashara ya samaki wachanga katika bwawa hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mhe. Aaron Yesaya Mbogho, ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya, amesema, pamekuwepo na operesheni ya mara kwa mara katika bwawa hilo.
Akiwa anazungumzia zoezi la kuwakamata wahalifu waliokamatwa usiku wa kuamkia leo, ameeleza kuwa, zoezi la kuwakamata wahalifu hao limefanyika kuanzia saa nne usiku mpaka saa saba usiku. Ametabainisha kuwa, ofisi yake kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama Wilaya pamoja na wataalam wa uvuvi wa Halmashauri, wamewakamata watuhumiwa sugu wa uvuvi haramu na wafanya biashara ya samaki wachanga watatu ambao ni, Godlizen B. Mfinanga, Juma Hassani Muharuma na Shafi B. Konde ambapo wengine walifanikiwa kukimbia. Watuhumiwa hao wamekamatwa wakiwa wamebeba ndoo 150 za samaki wachanga pamoja na nyavu haramu.
Pia katika operesheni hiyo wameweza kukamata magari mawili yote yakiwa ni aina ya pajero, moja likiwa na namba T 527 AEQ na lingine likiwa na namba T 210 ADF. Pia wamekamata pikipiki mbili zenye namba za usajili MC 546 CBR na MC 527 BPV.
Akizungumza kuhusu zoezi hili, Afisa Uvuvi Ndg. David Kabodo alisema, operesheni ya uvuvi haramu katika bwawa la Nyumba ya Mungu ni endelevu na watakwenda mpaka Wilaya ya Simanjiro husasani kwenye vijiji vinavyozunguka bwawa ili kuhakikisha kuwa, wavuvi haramu wanaokimbilia huko wanatiwa mbaroni na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Aidha, ofisi ya Mkuu wa Wilaya inaendelea kutoa wito kwa wananchi wa Wilaya zinazo zunguka bwawa hilo kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa serikali ili uvuvi haramu uweze kutokomezwa. Pia ofisi inaendelea kutoa shukrani kwa wananchi wanaoendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa pale wanapo ona vitendo vya uvuvi haramu katika maeneo yao.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa