Na Angela Msimbira OR-TAMISEMI.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa amepiga marufuku walimu kupita kila Ofisi ya Halmashauri kutafuta huduma na ameagiza wapelekewe huduma hizo shuleni badala ya watoa huduma kufatwa. Ofisini.
Ametoa agizo hilo leo tarehe 8 Septemba, 2022 Jijini Dodoma wakati akiongea na waandishi wa habari kutoa taarifa kwa umma ya uboreshaji wa huduma kwa walimu nchini.
“Ni marufuku kuwaacha walimu kupita kila ofisi ya Halmashauri kutafuta huduma, narudia tena mwalimu apelekewe huduma shuleni badala ya watoa huduma kukaa ofisini” amesema Bashungwa
Amesisitiza kuwa Mwalimu akiandika barua kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhitaji huduma, anapaswa kujibiwa kwa maandishi ndani ya siku 7 baada ya kupokelewa.
Aidha, Bashungwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote nchini kuwasimamia Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Maafisaelimu, Maafisa wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Wathibiti Ubora wa Shule kuhakikisha wanawafuata walimu mashuleni na kutatua kero na malalamiko yao kwa wakati.
Amewataka viongozi hao kufuatilia na kuwasimamia viongozi wa elimu katika ngazi ya Mikoa, Halmashauri, Kata na shule kutekeleza mikakati ya uboreshaji na usimamizi wa elimu na kuhakikisha wanawasilisha taarifa ya utekelezaji Ofisi ya Rais – TAMISEMI kila robo mwaka.
Vile vile, amewataka kusimamia utekelezaji wa Mipango ya Mafunzo kazini kwa walimu, kwa mujibu wa Mwongozo uliotolewa na Katibu Mkuu Utumishi na ufanyike kwa uwazi na ushirishwaji wa kutosha, ili kuondoa dhana ya kuwa waajiri wanatoa nafasi za mafunzo kwa upendeleo.
Pia, Bashungwa amewaelekeza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwasimamia Maafisa wa Tume ya Utumishi wa Walimu kuzingatia miongozo ya upandishwaji vyeo walimu, ili kila anayestahili kupandishwa cheo, anapandishwa kwa mujibu Sheria, Kanuni na Miongozo.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa