Leo, Waziri wa Wizara ya Maji Prof. Makame Mbarawa (Mb) amezuru Wilaya ya Mwanga na kuwahakikishia wananchi wa Mwanga kuwa, siku siyo nyingi watapata maji ya kutosha kutoka kwenye mradi mkubwa wa maji unaojengwa kwa sasa, mradi ambao utahudumia Wilaya mbili za Mkoa wa Kilimanjaro ambazo ni Mwanga na Same na wilaya moja ya Mkoa wa Tanga ambayo ni Korogwe.
Mradi huo ambao unafahamika kwa jina la Same - Mwanga - Korogwe, ambao chanzo chake ni Bwawa la nyumba ya Mungu lililopo Wilayani Mwanga, una thamani ya shilingi Bilioni 241 na unatarajiwa kunufaisha takribani wananchi 434,000 wa wilaya zote tatu (Mwanga, Same na Korogwe).
Katika ziara yake hiyo, Mhe. Prof. Mbarawa amesema kwamba, kuna baadhi ya sababu zinazopelekea mradi kuchelewa kukamilika ikiwa ni pamoja na ucheleweshwaji wa vifaa katika bandari ya Dar es Salaam. Mhe. Waziri amewaahidi wasimamizi wa mradi kuwa, atafuatilia kwa haraka vifaa vilivyokwama bandarini ili viweze kutoka na kazi iendelee kwa kasi.
Aidha, akiwa katika kuhitimisha ziara yake Wilayani Same, Mhe. Waziri amesema, Vijiji vyote vilivyopitiwa ama vilivyoko kandokando na mradi wa maji vitapatiwa maji, na sasa wataalamu wameshapewa jukumu na Serikali kuandika andiko kwa ajili ya Vijiji ambavyo awali vilikuwa havijajumuishwa kwenye mradi.
Ili kuhakikisha kuwa zoezi la kukamilisha mradi huo linakwenda kwa haraka, Mhe. Waziri amemwagiza Mkandarasi wa mradi kuhakikisha kuwa, wanaajiri wakandarasi wengine (sub contractors), ili kuifanya kazi iende kwa haraka na kukamilika kwa wakati. Amesema kwamba, mpaka sasa kasi ya mkandarasi siyo ya kuridhisha, na Serikali kuanzia sasa haitafumba macho kama kasi ya mradi itakwenda ndivyo sivyo.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa