Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga kupitia Idara ya Elimu Sekondari, kuanzia muhula wa kwanza wa mitihani wa mwezi Juni 2018, itakuwa na mtihani mmoja unaofanana kwa Wilaya nzima, kuanzia kidato cha kwanza, hadi kidato cha sita. Utaratibu huu wa kufanya mtihani wa mfanano kwa shule zote za Wilaya, utakuwa endelevu na utafanyika kwa mihula yote kwa kila mwaka.
Akizungumza kwenye kikao kazi na Wakuu wa shule za Sekondari za Serikali na binafsi, Afisa Elimu Sekondari Ndg. Chacha Megewa amesema mtihani huo utajumuisha shule zote za binafsi na za serikali. Amesema kuwa lengo kubwa la kuja na mpango huo ni ili kuinua taaluma ndani ya Wilaya ya Mwanga na kuifanya Wilaya iwe juu zaidi kimkoa na kitaifa. Pamoja na kuwa mtihani huo utachangia kuinua kiwango cha taaluma, pia utakuwa na faida kwa kuleta ushindani kati ya shule na shule, kuimarisha kiwango cha ufaulu, kuimarisha na kuendeleza vipaji, kuwezesha shule kumaliza muhtasari kwa wakati na itasaidia kutatua changamoto za kitaaluma kwa karibu zaidi.
Katika kuhakikisha kuwa mpango huo unakuwa na manufaa, Ndg. Chacha aliunda timu maalum iliyokwenda Jijini Arusha na kujifunza ni kwa namna gani Jiji hilo lilivyoweza kulisimamia jambo hilo na kuweza kuwa la manufaa kwa shule zake kwani, Jiji la Arusha, ndio walioanza mpango huo na umeonekana kuwa, utakuwa na manufaa sana kwa shule za Wilaya ya Mwanga.
Nao Wakuu wa shule wamelipokea jambo hili kwa furaha, na kusema kuwa wapo tayari kulifanyia kazi kwa kuonyesha ushirikiano kwa asilimia mia moja. Wakuu wa shule hao wamesisitiza kuwa maoni yatakayowasilishwa kwao na kamati iliyoteuliwa, ambapo maoni hayo yatakuwa yanaeleza namna ya kuendesha mtihani huo, watakuwa tayari kuyafanyia kazi mawazo ya kamati na watayasimamia ili kuhakikisha mtihani huo unafanyika kama walivyokubaliana.
Samba na hilo, Afisa Elimu Ndg Chacha, alitumia kikao kazi hicho, kuwakumbusha Wakuu wa shule kuhusu namna ya kuendelea kuwa na utendaji kazi bora, kwa kipindi hiki cha serikali ya awamu ya tano. Amewaonya baadhi ya Wakuu wa Shule kuzembea kuleta taarifa za miradi ya ujenzi ofisini kwake. Akiongea kwa msisitizo Ndg Chacha alisema, haiwezekani mradi upo shuleni kwako na taarifa huleti ofisini kwangu, badala yake unasubiri hadi nikuombe taarifa hizo. Amesema taarifa ni vizuri azione kwasababu lengo la taarifa ni kuonyesha uwazi, na hii itaepusha kutiliwa shaka kwenye mradi husika.
Kuhusu suala la maendeleo ya shule, Ndg Chacha amesisitiza, ili shule ziweze kufanya vizuri ni lazima Wakuu wa shule wahakikishe wanafunzi wanapatiwa chakula cha mchana, na amewasisitiza Wakuu wa shule kuhakikisha wanalisimamia vizuri suala hili kwa kuwashirikisha wazazi, Watendaji wa Kata, Watendaji wa Vijiji na Waratibu Elimu Kata. Ameendelea kusema kuwa, kwa shule ambayo haina bodi, kuanzia sasa bodi ianzishwe kwani haiwezekani shule kuendeshwa bila bodi. Pia amekemea tabia ya baadhi ya walimu kutembea na wanafunzi na hata wakati mwingine kuwapa mimba. Amewaagiza Wakuu hao kuhakikisha wanasimamia nidhamu za walimu na wanafunzi wao ili waweze kuboresha elimu kwenye shule wanazo zisimamia.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa