Leo Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga imeadhimisha sikukuu ya Miaka 59 ya Muungano kwa kufanikiwa kupanda zaidi ya miti 200 katika eneo ambalo hospitali mpya ya Wilaya ya Mwanga inaendelea kujengwa. Sikukuu ya Muungano kwa mwaka huu imebebwa na kuli mbiu inayo sema “Umoja na Mshikamano Ndiyo Nguzo ya Kukuza Uchumi Wetu”.
Zoezi hilo la upandaji miti limeongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Mhe. Abdallah Mwaipaya kwa kushirikiana na watumishi mbalimbali wa umma, Viongozi wa Chama tawala, wananchi na wanafunzi.
Akiongea wakati wa zoezi hilo la upandaji miti Mhe. Mkuu wa Wilaya amesema kwamba, suala la utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji ni ajenda kuu ya Kitaifa, hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha kwamba analinda na kutunza mazingira na vyanzo vya maji. Zoezi la upandaji miti katika Wilaya ya Mwanga ni zoezi ambalo ni endelevu, tutaendelea kupanda miti kwenye taasisi zetu za umma ili mazingira yaendelee kuwa mazuri, amesema Mhe. Mkuu wa Wilaya. Amewaasa wananchi kuhakikisha kwamba miti ambayo imepandwa leo na miti mingine ambayo ilikwisha pandwa awali katika eneo hilo la hospitali ya Wilaya, inaendelee kulindwa na kutunzwa vizuri.
Aidha, Mhe. Mkuu wa Wilaya amesema kwamba, kuna faida nyingi za utunzaji wa mazingira ikiwa ni pamoja na biashara ya hewa ukaa ambayo itasaidia katika kukuza mapato ya serikali. Faida nyingine ni pamoja na hali ya hewa nzuri, mvua za kutosha, vyanzo vya kudumu vya maji na mazingira bora ya viumbe hai.
Mhe. Mkuu wa Wilaya amewataka wananchi wa Mwanga haswa wafugaji kuhakikisha kuwa wanalinda na kutunza mifugo yao vizuri, ili kuepuka kuingia kwenye mgogoro na serikali, pale mifugo yao itakapo haribu miti na mazingira haswa kwenye maeneo yote ambapo serikali imepanda miti na maeneo yote yaliyo hifadhiwa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Bi. Mwajuma A. Nasombe amesema kwamba, kwa mwaka huu, Halmashauri ya Mwanga imepanga kupanda miti zaidi ya elfu kumi. Zoezi hilo la upandaji miti lilisha anza ambapo kila shule na taasisi zingine za umma zimehimizwa kupanda miti ili kutunza mazingira.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huwa inaadhimisha sikukuu ya Muungano kila inapo fika tarehe 26 Aprili ya kila mwaka, lengo likiwa ni kumbukizi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambapo, Tanganyika na Zanzibar ziliungana mnamo tarehe 26 Aprili, 1964.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa