Katika kuelekea maadhimisho ya siku 16 za kupinga vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake na watoto, leo Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, kwa kushirikiana na taasi ya Yatosha Foundation ya Wilayani Mwanga, imeadhimisha siku ya kupinga vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto.
Maadhimisho hayo, ambayo yalianza kwa maandamano yaliyo ongozwa na, wanafunzi zaidi ya 500 wa shule za msingi Mramba, Kawawa na Lwami, yalipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Mhe. Abdallah Mwaipaya katika uwanja wa C. D Msuya.
Maadhimisho ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto, ambayo yalibebwa na kauli mbiu inayosema “Kila Uhai Una Thamani, Tokomeza Mauaji na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto”, yalilenga kufikisha ujumbe kwa jamii na kutoa elimu juu ya vitendo vya kikatili vinavyofanywa kwa wanawake na watoto. Vitendo hivi vimekuwa vikileta maumivu makali ya kimwili na kiakili kwa wahusika na hata kupelekea msongo wa mawazo kwa wanaofanyiwa vitendo hivyo.
Mgeni rasmi katika tukio hilo ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, amesema kwamba, kuna haja kubwa kwa jamii ya watu wa Mwanga, kuendelea kupatiwa elimu ya mara kwa mara juu ya umuhimu wa kulinda na kutetea haki za watoto pamoja na wanawake, ili, kuwaepusha na vitendo vya kikatili, ambavyo wamekuwa wakifanyiwa mara kwa mara. Amesisitiza kwamba, wazazi nao wahakikishe kuwa, wanatoa nafasi ya kuwasikiliza watoto wao, kwani watoto wengi wakifanyiwa vitendo vya kikatili, baadhi ya wazazi hawana muda wa kuwasikiliza.
Katika hotuba yake, Mhe. Mkuu wa Wilaya ameendelea kusema, elimu dhidi ya ukatili isiishie kutolewa na watu wachache tu, bali iendelee kutolewa kupitia taasisi na mashirika mbalimbali ya binafsi na serikali ili watoto waelewe haki zao za msingi na waweze kujua ni namna gani ya kuepuka au kutoa taarifa dhidi ya mambo ya kikatili ambayo wamekuwa wakifanyiwa nyumbani ama mtaani.
Aidha, Mkuu wa Wilaya, hakuacha kuzungumzia juu ya umuhimu wa chakula cha mchana shuleni kwa kusema, “Serikali ya Wilaya ya Mwanga itaendelea kuwaelimisha wazazi, juu ya umuhimu wa chakula cha mchana shuleni, na baada ya muda, wazazi ambao watakaidi, Serikali itabidi iwachukulie hatua kwasababu, suala la kumnyima mtoto chakula cha mchana, ni sehemu ya unyanyasaji na ukatili” Amesema Mkuu wa Wilaya. Ametoa wito kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Bi. Mwajuma Nasombe kwa kusema, shule zote za Wilaya ya Mwanga zianzishe Club maalum za kupinga ukatili dhidi ya watoto, kwani hii itasaidia kubaini mambo mengi ya kikatili wanayofanyiwa watotoi na namna ya kukababiliana nayo.
Maadhimisho ya siku ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, ni zoezi la kitaifa ambalo lilianza toka tarehe 25 Novemba, 2022, na yataazimishwa kwa muda wa siku 16 ambapo, hitimisho kitaifa itakuwa tarehe 10/12/2022.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa