Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga inategemea kupokea jumla ya wanafunzi 2700 wa kidato cha kwanza kwa mwaka 2023. Hayo yamesemwa leo tarehe 14.12.2022 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mwanga Bi. Mwajuma A. Nasombe, alipokuwa akizungumza kwenye ziara ya kukagua madarasa mapya ya kidato cha kwanza, iliyofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu, Wilayani Mwanga. Amesema kwamba, Halmashauri ya Mwanga ilipokea kiasi cha Tsh. Milioni 180 kutoka Serikalini kwa ajili ya ujenzi wa jumla ya madarasa mapya tisa. Madarasa hayo kwa sasa yamekamilika na tunachosubiri ni kupokea jumla ya wanafunzi 2700 wa kidato cha kwanza ili waweze kusoma, amesema Bi. Nasombe.
Akiwa katika ukaguzi wa madarasa hayo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu, amesema kuwa, ameridhishwa sana kwa kazi nzuri illiyofanywa na viongozi wote wa Wilaya ya Mwanga, kwa kushirikiana na wananchi kwa kuhakikisha kwamba, ujenzi wa madarasa hayo unakamilika kwa wakati. “Madarasa yaliyojengwa ni mazuri sana, niwaombe tuyalinde vizuri na tuyatumie kwa ajili ya wanafunzi wetu, alisema Mkuu wa Mkoa’’. Akitoa pongezi kwa Serikali, Mhe. Babu alisema, anamshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Mwanga fedha za ujenzi wa madarasa hayo.
Mhe. Mkuu wa Mkoa ameendelea kusema, wanafunzi wote watakaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza 2023 katika Mkoa wa Kilimanjaro, hakuna mwanafunzi hata mmoja atakayeshindwa kujiunga na masomo kutokana na ukosefu wa madarasa kwasababu, madarasa yaliyopo yanatosha kuwapokea wanafunzi wote watakaokuwa wamechaguliwa. Amewaagiza wazazi wote kuhakikisha kwamba, wanafunzi watakaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza 2023, wanakwenda shuleni. Amisisitiza kwamba, kuanzia juma la pili baada ya shule kufunguliwa atatembelea shule na kukagua kama wanafunzi wamefika kwa ajili ya kuanza masomo.
Wilaya ya Mwanga ilipokea kiasi cha fedha Tsh. Milioni 180 mwanzoni mwa mwezi Octoba, 2022 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa tisa. Shule zilizonufaika na fedha hizo ni pamoja na Shule ya Sekondari Kifaru madarasa mawili, Shule ya Sekondari Usangi Day madarasa mawili, Shule ya Sekondari Kwangu madarasa mawili, shule ya Sekondari Mgagao, madarasa mawili na shule ya Sekondari Vudoi Darasa moja. Madarasa hayo yameshakamilika yakiwa na viti pamoja na meza zake.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa