Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira imewaeleza wananchi wa Kijiji cha Ruru, Kata ya Jipe Wilayani Mwanga kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bado inaendelea kulichukulia kwa uzito tatizo la magugu maji linalo kabili ziwa Jipe lililopo Wilayani Mwanga.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. Khamis H. Khamis (Mb) leo tarehe 10 Agosti, 2023, alipo tembelea ziwa Jipe kwa lengo la kuona namna ambavyo magugu maji yameathiri ziwa hilo.
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ruru, Mhe. Naibu Waziri amesema kwamba, Serikali bado inatambua changamoto ya magugu maji ya ziwa Jipe na itahakikisha kuwa, magugu maji hayo yanaondolewa kwani mpaka sasa serikali imesha andika andiko lenye thamani ya fedha za kitanzania shilingi bilioni 18 na kuwasilisha kwa wahisani ili waweze kufadhili mradi wa kuondoa magugu maji hayo. Amewahakikishia wananchi hao kwamba, mara fedha hizo zitakapo patikana, serikali itaanza mradi huo mara moja.
Pamoja na hayo, Mhe. Naibu Waziri, amewataka wananchi wa Kata ya Jipe na maeneo yote yanayo zunguka ziwa hilo, kuhakikisha kwamba, wanatunza mazingira ili kuepuka athari za mabadiliko ya tabia nchi, ikiwa ni pamoja na ukame wa muda mrefu. Amewataka wananchi hao kupanda miti ya kutosha pamoja kuepuka kufanya shughuli za kibinadamu pembezoni mwa ziwa hilo.
Ziwa Jipe ni ziwa ambalo lipo limezungukwa na nchi ya Kenya na Tanzania na lina ukubwa wa kilomita za mraba 30KM2 na linasaidia maisha ya wananchi wa Tanzania wapatao 3222 kwenye shughuli za uvuvi, kilimo, ufugaji na uhifadhi wa bionuwai pamoja na shughuli za utalii.
Shughuli za uvuvi zimepungua kwa kiasi kikubwa kwenye ziwa hilo kutokana na magugu maji yaliyo ota ziwani haswa upande wa Tanzania. Hii imepelekea serikali kuhangaika kwa hali na mali, ili kuhakikisha kwamba, tatizo la magugu maji hayo linapatiwa ufumbuzi.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa