Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, jana iliendesha zoezi la kuogesha mifugo, zoezi ambalo uzinduzi wake ulifanyika katika kata ya Kileo.
Katika zoezi hilo ambalo lilizinduliwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri Ndg. Ezekiel Mwasumbi, jumla ya ng'ombe 577 walipatiwa huduma ya kuogeshwa.
Afisa Mifugo wa Kata ya Kileo, Ndg. Huseni Msemo, akiwa anasoma risala ya ufunguzi wa zoezi hilo, mbele ya Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, alisema, kuna faida nyingi ambazo wafugaji watazipata kutokana na mifugo yao kuogeshwa ikiwa ni pamoja na ng,ombe kupata dawa mwili mzima tofauti na kuogesha kwa bomba la mgongoni, kuzuia magonjwa mengi na kuondoa magonjwa mwilini.
Naye akizungumza mbele ya wafugaji walioleta mifugo yao kwa ajili ya kuogeshwa, Afisa Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Ndg. Emmanuel Sindiyo alisema Halmashauri ina jumla ya majosho 16 ambapo majosho 2 tu ndiyo mazima. Amesema, kwa mwaka mpya wa fedha 2019/20, Halmashauri inatenga bajeti kwa ajili ya kuboresha majosho. Afisa Mifugo huyo aliendelea kusema, kwa siku ya kwanza, mifugo 2,000 ya awali itaogeshwa bure na siku zitakazo fuata mifugo italipiwa gharama za kuogeshwa ambapo gharama itakuwa Tsh.600 kwa ng'ombe na Tsh. 100 kwa mbuzi mmoja.
Zoezi hili la kuogesha mifugo ni zoezi ambalo ni endelevu na la lazima. Kila mwananchi ambaye ni mfugaji, ni lazima ahakikishe kuwa anapeleka mifugo ili iogeshwe. Hii ni kwa mujibu wa sheria ya mifugo ya mwaka 203, alisema Afisa Mifugo na Uvuvi.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa