Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, jana tarehe 05 mei, 2021, ilitembelea miradi minne ya maendeleo iliyopo hapa Wilayani Mwanga. Katika miradi hiyo, miradi miwili ni ya afya na mingine miwili ni ya elimu.
Miradi ya afya iliyokaguliwa ni pamoja na mradi wa kituo cha afya Kigonigoni ambao una thamani ya Tsh. 440,551,415 na mradi wa afya Kisangara wenye thamani ya Tsh. 488,917,910.
Miradi ya elimu iliyotembelewa ni mradi wa maabara shule ya sekondari Kwangu, mradi ambao unahusisha ukarabati wa maabara. Thamani ya mradi huu ni Tsh. 35,432,000. Mradi mwingine wa elimu ni mradi wa ujenzi wa madarasa matatu, choo matundu saba na bweni moja katika shule ya msingi Kwamavusha. Mradi huu una thamani ya Tsh.155,159,000.
Sambamba na zoezi la utembeleaji wa miradi hiyo, kamati ilitoa maelekezo kuwa, mkataba wa kituo cha afya kigonigoni uvunjwe na kutafuta mafundi wengine kwani mafundi wameshindwa kumaliza kazi kwa wakati kwa mujibu wa mkataba. Kamati pia ilibaini uwepo wa upotevu wa vitasa 40 vya milango katika kituo hicho na kuagiza kuwa, Mkurugenzi Mtendaji amchukulie hatua za kinidhamu mtumishi aliyehusika na upotevu wa vitasa hivyo. Pia kamati ilibaini uwepo wa vifaa vilivyokwisha muda wa matumizi na kuagiza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mtumishi aliyehusika na ununuzi wa vifaa hivyo katika kituo hicho cha Kigonigoni.
Katika kituo cha afya Kisangara, kamati ilimuagiza Mwandisi wa Ujenzi Wilaya kwa kushirikiana na mkaguzi wa ndani Wilaya kuhakikisha kuwa, wanafanya tathmini upya ya gharama za kumalizia ujenzi wa njia ya wagonjwa (Walk Way) na gharama za umaliziaji wa jengo la kuhifadhia maiti na kufulia kisha kuwasilisha taarifa katika kamati ya fedha, uongozi na mipango. Pia Mkaguzi wa ndani ameagizwa kuwa, ahakikishe anafanya ukaguzi wa matumizi ya fedha zilizotumika katika mradi wa kituo hicho.
Kwa upande wa miradi ya elimu, kamati ilitoa pongezi kuwa, miradi ni mizuri na kazi inaridhisha. Aidha kamati ilitoa maelekezo kuwa, hatua ya umaliziaji iliyobaki kwenye miradi hiyo iende kwa wakati ili miradi ianze kutumika.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa