Jana tarehe 12 Februari, 2020, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dr. Faustine Ndugulile alifanya ziara ya kikazi Wilayani Mwanga na kuweza kutembelea Hospitali ya Wilaya Usangi na baadae kutembelea zahanati za Lembeni na Kileo.
Katika ziara yake hiyo, Dr. Ndugulile alifurahishwa kwa namna huduma mbalimbali zinavyoendeshwa katika hospitali ya wilaya, mathalani namna malipo yanavyofanyika, utunzaji wa kumbukumbu na uwepo wa madawa hospitalini hapo. Waziri hakuacha kuweka wazi namna alivyofurahishwa na njia nzuri ya ukusanyaji wa mapato kielekroniki ambapo njia hii imepelea mapato kuwa makubwa na kutoruhusu mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali. Mapato ya hospitali hiyo ambayo yanatokana na malipo ya papo kwa papo, NHIF na CHF kwa sasa yamefikia wastani wa milioni kumi kwa mwezi na yanategemea kuongezeka.
Aidha, Mhe. Waziri aliendelea kusisitiza kuwa, Serikali imetoa milioni mia nne kwa ajili ya hospitali hiyo na ametoa maelekezo kuwa, fedha hizo zifanye kazi ambayo ni ya kuonekana na inayoendana na thamani halisi ya fedha hizo.
Akielezea mikakati ya kuzitumia fedha hizo, Mganga Mfawadhi wa hospitali Bi. Upendo I. Shuma alisema, uongozi umeshakaa na kuona kwamba, kuna umuhimu wa kujenga majengo mapya matatu ambayo ni jengo la maabara, upasuaji na jengo la mama na mtoto. Mhe. Waziri aliridhishwa na mipango mizuri ya namna fedha hizo zitakavyotumika na kuongezea kwamba, zitumike vizuri na kama zitabaki, ziweze kufanya jambo lingine la kuonekana hospitalini hapo.
Sambamba na hayo, Dr. Ndugulile alitoa ushauri kuhusu zahanati za Lembeni na Kileo na kusema kwamba, zahanati hizi zinapaswa zikamilike kwa haraka ili wananchi waendelee kunufaika na huduma nzuri za matibabu zitakazokuwa zinatolewa katika zahanati hizo. Akiwa katika zahanati ya Lembeni, Mhe. Waziri alichangia mifuko 50 ya saruji ikiwa ni hatua ya kuunga mkono umaliziaji wa jengo jipya la zahanati hiyo. Katika zahanati ya Kileo, aliagiza kwamba, ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya na Mkoa wakae na kuweka mikakati mizuri ya namna ya kuendeleza mradi mpya wa jengo la zahanati ya Kileo. Pia alimwagiza mganga mfawidhi wa kituo hicho kuhakikisha kwamba, sehemu ya mapato yanayopatikana katika zahanati hiyo, yanafanya ukarabati mdogomdogo kwenye jengo la zahanati linalotumika kwa sasa.
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga
Sanduku la Posta: 176 Mwanga,Kilimanjaro
Simu ya Mezani: +255 272974343
Namba ya Simu: +255 272974343
Barua Pepe: ded@mwangadc.go.tz
hatimiliki ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga . Haki zote zimehifadhiwa